JAJI MKUU AWATAKA WATUMISHI WA MAHAKAMA KUTUMIA TAKWIMU KUJITATHMINI
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka watumishi wa Mahakama nchini kutumia takwimu kujitathmini utendaji kazi wao.
Akizungumza na watumishi wa Mahakama Kanda ya Dodoma wakati wa Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na watumishi hao, Jaji Mkuu pia alisisitiza umuhimu wa Maafisa wa Mahakama kutumia takwimu sahihi katika utekelezaji wa mipango na shughuli mbalimbali za Mahakama.
Akielezea faida za matumizi ya takwimu kwa watumishi wa Mahakama, Jaji Mkuu alisema takwimu zinasaidia watumishi kujitathmini utendaji kazi wao pamoja na kufanya maboresho ya huduma za utoaji haki.
Alizitaja faida nyingine za matumizi ya takwimu sahihi kuwa ni pamoja na kupata mrejesho wa huduma zinazotolewa na kufanya maboresho. Alisema kwa kutumia takwimu, Mahakama moja inaweza kujilinganisha na nyingine na kujua ni maeneo gani yanafanya vizuri na changamoto ni zipi.
“Takwimu ndiyo inakupa undani wa changamoto, mafanikio na pia unaweza kutumia kufanya maboresho ya huduma, takwimu zinasaidia kujirekebisha badala ya kusubiri wananchi kulalamika ndiyo tufanye marekebisho”, alisisitiza Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu alielezea umuhimu wa matumizi sahihi ya takwimu kufuatia kufurahishwa na Taarifa ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kuhusu hali ya mashauri kuanzia Januari 1 hadi Agosti 30, 2022 iliyokuwa imesheheni takwimu zinazoweza kutumiwa na Mahakama katika kujitathmini utendaji wake.
Kwa upande wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani pia alisisitiza umuhimu wa matumizi ya takwimu sahihi katika kufanya maamuzi ndani ya Mahakama.
“Ili tufanye maamuzi sahihi kwa kutumia takwimu ni lazima tuwe na takwimu, alisema Jaji Kiongozi.
Jaji Kiongozi pia amewaagiza Naibu Wasajili wote nchini kuhakikisha mfumo wa kusajili mashauri na taarifa ujulikanao kama JSDS ll unatoa takwimu sahihi za mashauri ili Mahakama iwe na takwimu sahihi zitakazosaidia katika kufanya maamuzi mbalimbali.